Wednesday, March 6, 2013

MABIBO BEER WINE AND SPIRIT WATAHADHALISHA WAFANYABIASHARA WANAOINGIZA BEER YA WINDHOEK KINYUME CHA SHERIA

KAMPUNI ya Mabibo Beer Wines and Spirits Ltd, imewahimiza wafanyabiashara wenye bia za Windhoek zilizoingizwa nchini bila kulipa ushuru, wazipeleke katika ofisi za kampuni hiyo ili wasamehewe na kupewa bia nyingine. Ushauri huo umetolewa jijini Dar es Salam na Mshauri wa Kimataifa wa kujitegemea katika masuala ya Kibiashara, James Rugemalila. “Nayasema haya kwa sababu hivi karibuni, Kampuni ya Mabibo Beer Wines and Spirits Ltd, iliwabaini wafanyabiashara wanaofanya utapeli wa kuingiza Windhoek Premium Lager Beer isiyo na code namba MB66. “Wafanyabiashara hao wadanganyifu wanakwepa kodi za Serikali, hali inayoikosesha Serikali mapato yake na kupunguza uwezo wa Serikali wa kuihudumia jamii,” alisema Rugemalila. Rugemarila alisema kwamba, kampuni hiyo ndiyo pekee iliyopewa leseni halali ya kuagiza na kusambaza kinywaji cha Windhoek Premium Lager Beer nchini Tanzania na ili kutambulisha uingizaji halali wa kinywaji hicho, Mabibo huweka alama yenye code namba MB66 kwa bia zote za Windhoek zinazoingizwa Tanzania kihalali. “Kwa hiyo, bia zote za Windhoek zinazoingizwa nchini zenye code namba MB66 ndiyo bia halali, pia ndiyo utambulisho wa uhakika kuwa bia hizo kwani zimelipiwa ushuru na kodi nyingine za Serikali na ili kuufanya utaratibu huu wa kufanya biashara halali uwe na nguvu ya kisheria, Kampuni ya Mabibo Beer Wines and Spirits Ltd, iliwasilisha vielelezo vyote halali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kinondoni Dar es Salaam na kuiomba Mahakama itambue kwa mujibu wa sheria haki hiyo ya kibiashara ya Kampuni ya Mabibo,” alisema Rugemarila. Alisema baada ya kuridhika na vielelezo vyote halali vilivyowasilishwa na kampuni kuwa Mabibo ndiyo kampuni pekee yenye leseni ya kuagiza na kusambaza kinywaji hicho cha Windhoek Premium Lager Beer, Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni Dar es Salaam, ilitoa amri ya kuzuia na kulifanya kosa la jinai kwa mtu yeyote kuuza bia ya Windohoek isiyo na code namba MB 66 bila kibali halali cha maandishi kutoka Kampuni ya Mabibo Beer Wines and Spirits Ltd. Aidha, alisema faida za kufuata taratibu halali za kufanya biashara ni nyingi, lakini faida muhimu ni kuwa mlaji anapata kinywaji ambacho ni salama kwa sababu chanzo chake kinajulikana na pia njia za usafirishaji ni salama kwa sababu mhusika anatambulika kisheria.

No comments:

Post a Comment