Tuesday, November 28, 2017

MEYA IRINGA NA MAKADA WATANO CHADEMA WAFIKISHWA MAHAKAMANI


Meya wa Manispaa ya Iringa Alex Kimbe mwenye koti la suti akitolewa mahabusu kwenda mahakamani kusikiliza kesi ilitolewa ikimkabili ya kutishia kuua kwa bastola 
Meya kushoto akiwa chini ya ulinzi
MSTAHIKI meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa Alex Kimbe (chadema) amepandishwa mahakamani kwa kosa la kutishia kumuua katibu wa UV CCM wilaya ya Iringa mjini Alphonce Myinga wakati wa zoezi la uchaguzi mdogo wa udiwani kata ya Kitwiru.

Meya Kimbe alifikishwa mbele ya hakimu mkazi wa mahakama ya wilaya ya Iringa John Mpitanjia leo majira ya saa 3 asubuhi na kusomewa shitaka hilo la jinai kesi namba 189 /2017.

Akisoma shitaka hilo wakili wa jamhuri Allysniki Mwinyiheni alisema kuwa Kimbe alitenda kosa hilo Novemba 26 mwaka huu katika eneo la Kitwiru mjini Iringa kwa kumtishia kumuua kwa bastola Myinga .

Hata hivyo Kimbe alikana kosa hilo na kesi hiyo kuja tena mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa Desemba 12 mwaka huu na meya huyo yuko nje kwa dhamana baada ya mahakama kukubali kumpa dhamana .

Wakati huo huo makada watano wa Chadema jana walifikishwa mbele ya hakimu mkazi mwandamizi wa mahakama ya mkoa wa Iringa Richard Kachele kwa makosa matatu likiwemo la unyang’anyi .

Wakili wa jamhuri alisema mahakamani hapo kuwa washitakiwa hao Martha Robarth , Leonard Kulujila, Christopher Gerlad,Samweli Nyanda na Asau Bwile kwa pamoja wanashitakiwa kwa makosa matatu ambayo ni kujeruhi, Unyang’anyi wa kutumia nguvu na utekaji .

Kuwa tukio hilo walilifanya Novemba 19 mwaka huu eneo la Kitwiru kwa kumteka Dikri Frank kada pamoja na kumteka walimpokonya simu yake ya mkononi yenye thamani ya shilingi 100,000 pamoja na kadi ya CCM moja.

Washitakiwa hao ambao wanatetewa na wakili CHarzy Luoga walikana kosa hilo na kunyimwa dhamana kutokana na kosa la unyang’anyi katika kesi hiyo namba 190/2017 kutokuwa na dhamana .

Wakili wa washitakiwa hao aliiomba mahakama kuagiza wapelelezaji wa kesi hiyo kufanya haraka kwani wateja wake wana maumivu na mmoja hawezi hata kusimama baada ya kuumizwa na polisi wakati walipokamatwa .

Kesi hiyo imeahirishwa hadi Desemba 12 mwaka huu itakapofikishwa tena kwa ajili ya kutajwa na washitakiwa wote walirudishwa mahabusu