Sunday, August 11, 2013

SOMA TUKIO ZIMA LA SHEKH PONDA KUPIGWA RISASI NA POLISI MOROGORO


Shekh Ponda akisisistiza jambo mbele ya waumini wa Dini ya Kiislamu, wakati akizungumza kwenye Kongamano, jana mjini Morogoro.
Shekh Ponda akisisistiza jambo mbele ya waumini wa Dini ya Kiislamu, wakati akizungumza kwenye Kongamano, jana mjini Morogoro.
 Askari wa FFU wakijisogeza kati kati ya uwanja mara baada ya muda wa kongamano kumalizika.
Shekh Ponda, akitambulishwa jukwaani.
 Kikosi cha FFU uwanjani.
 Shekh Ponda akiteta jambo na baadhi ya Viongozi wa umoja wa Wahadhiri wa Dini ya Kiislamu Mkoa wa Morogoro, baada ya kuona magari ya askari yakisogea katikati ya uwanja.
Shekhe Ponda akiwa amezingirwa na waumini
*******************************************

*SHEKHE PONDA ALIPOTOROSHWA NA MASHEIKH KATIKA JARIBIO YA KUTIWA NGUVUNI NA POLISI MORO.

Na John Nditi, Morogoro. 
 KATIBU wa Jumuiya ya Kiislamu nchini , Shekhe Ponda Issa Ponda, jana jioni alijikuta katika wakati mgumu baada ya kuumizwa na kitu kinachodhaniwa kuwa ni risasi kwenye bega lake la kulia wakati akiekelea katika Msikiti wa Mungu Mmoja Dini Moja wa Mjini Morogoro baada ya kumalizika kwa kongamano ya Dini ya Kiislamu.
Mkasa huyo ulitokea majira ya saa 12: 15 za jioni eneo la barabara ya Tumbaku karibu na Fire, mara baada ya kumaliza kwa Kongamano hilo lililofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja Cha Ndege, Kata ya Saba Saba , Manispaa ya Morogoro.

Shekhe  Ponda alishiriki katika Kongamano hilo lililoandaliwa na Umoja wa Wahadhiri wa Dini ya Kiislamu Mkoani Morogoro na kufanyika siku ya Idd Pili kuanza saa nane mchana hadi kumi na mbili jioni ya siku hiyo. 
 Kongamano hilo lilipata baraka zote kutoka Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro, ambalo lilitoa  masharti kadhaa ya kuzingatiwa na wazungumzaji ikiwa ni kutokashifu dini nyingine wala viongozi wa serikali. 
 Sakata la kutaka kutiwa mbaroni kwa Shekhe Ponda lilikuja baada ya yeye kudaiwa kukiuka masharti ya Mahakama aliyopewa baada ya kuhukumiwa kifungo cha mwaka mmoja nje na  kutakiwa kutotenda kosa lolote wakati akitumikia adhabu hiyo.
 
 Mwenyekiti wa Kamati ya Maadalizi ya Kongamano hilo, Ustaadhi Idd Msema, alidai kuwa ''Shekhe Ponda baada ya kutoka ndani ya gari eneo la Uwanja wa Shule ya Msingi Kiwanja Cha Ndege, alipofika mita chache katika barabara ya Tumbaku alitelemka na wakati akitaka kuingia tena garini ilifyuliwa risasi iliyompiga begani''.  alisema Idd

 Ustaadh Msema aliongeza kuwa baada ya kupigwa risasi begani waumini waliokuwa wameambatana naye walimchukua na kumpakiza kwenye Piki Piki hadi Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro ili kupatiwa matibabu. 

 Kwa mujibu wa Mwenyekiti huyo, baada ya kufika hospitali, waliona anacheleweshwa kupatiwa matibabu na ndipo walipoamua kumwondoa na kumpeka kwenye Hospitali binafsi ambayo hakupenda kuitaja kwa jina. 

Akizungumzia kwa kina hali ya Shekhe Ponda baada ya kujeruhiwa, alisema kuwa yu hai licha ya kuumia vibaya begani na kwamba wanatarajia kumpekela eneo jingine hususani Jijini Dar es Salaam kupata matibabu zaidi.

Alisema viongozi wa Umoja huo hawawezi kuweka wazi sehemu anakotibiwa kwa kuwa jambo hilo ni la kiusalama zaidi hasa wakati huu ambapo kumekuwa na sinto fahamu.

Baadhi ya walinzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Morogoro waliozungumza juu ya tukio hilo , walikiri kuwa Shekhe Ponda alifikshwa hosptalini hapo kwa usafiri wa Piki piki zikiambatana na nyingine zaidi ya 50 na kuishia getini. 

 Walisema walimwingiza adi mapokezi na kwamba walipoona umati mkubwa upo getini waliamua kutoa taarifa Polisi kuwa wamevamiwa na watu, ambapo muda si mrefu Polisi wa FFU waliwasili na gari lao Hospitalini hapo. 

 Hata hivyo walinzi hao walisema, baada ya kuona Askari wamefika Hospitalini hapo, baadhi ya wafuasi wa Shekhe Ponda waliamua kumyanyua na kumbeba mabegani na kutoka naye mlango mwingine wakimlazimisha mlinzi kuwafungulia mlango na baadaye wakatokomea naye kwa usafiri wa Pikipiki kusikojulikana. 
Kufikishwa kwa Sheshe Ponda katika Hospitali ya Rufaa kulithibishwa pia na Mwenyekiti huyo ambaye alidai  kuwa waliamua kumwondoa baada ya kucheewa  kupatiwa huduma. 

Baada ya tukio hilo, uvumi ulisambaa meneo mbalimbali nchini ukidai kuwa Shekhe Ponda amepigwa risasi na Polisi na kufariki dunia. Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Morogoro, Feustine Shilongine akizungumza na Mwandishi wa Habari hizi majira ya saa tatu usiku wa Augosti 10, baada ya kutokea kwa tukio hilo, alisema kuwa hapakuwa na taarifa juu ya kutokea kifo cha Shekhe Ponda. 
 “ Nimepingiwa simu zaidi ya 50 , zikiulizia jambo hili...kuwa Ponda amefariki dunia ...Binafasi nami ninazisikia , ujumbe umesambazwa kwenye simu za watu mbalimbali...tumezunguka kila mahali hakuna kifo wala maiti yake ...na vijana wangu wanaendelea kulifuatilia suala hili” alisema Kamanda huyo. 

Mwenyekiti wa Kamati hiyo aliweka wazi kwa kusema kuwa Shekhe Ponda yu hai isipokuwa ameumia vibaya sehemu ya bega . 
 “ Nipo katika eneo ambalo Shekhe Ponda anapatiwa matibabu...sehemu ambayo hatuwezi kupataja kiusalama , isipo kuwa ameumia vibaya kwenye bega lake. Lakini yu hai wala hajafa” alisema Msema. Polisi Mkoani hapa bado haijatoa taarifa rasmi kuhusiana na sakata hilo, nasi twaendelea kufuatulia kwa ukaribu.

No comments:

Post a Comment