Sunday, October 27, 2013

MKUU WA MKOA WA DODOMA DR REHEMA NCHIMBI ASISITIZA MAADILI MEMA KWA WANAFUNZI MASHULENI.

Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi ametoa wito kwa shule zinazomilikiwa na taasisi za dini kuhakikisha zinaziba mianya yote ya mafundisho yasiyofaa kwa wanafunzi yanayoletelezwa na mabadiliko ya utandawazi ili ziweze kuzalisha wanafunzi wenye ubora kielimu na kimaadili.

Dr. Nchimbi alibainisha kuwa hivi sasa kumekuwa na mianya mingi inayowezesha mafundisho mbalimbali yanayopatikana kpitia maendeleo ya utandawazi ambayo baadhi yamekuwa na viashiria vinavyochangia kuharibika kwa tabia, maadili na mfumo mzima wa wanafunzi kujifunza na kuwaasa wanafunzi kuwa makini sana na masuala ya utandawazi katika safari zao za masomo kwani wasipotumia utandawazi ipasavyo itachangia kuharibikiwa katika masomo yao.

Dr. Nchimbi aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati wa mahafali ya tisa ya sekondari ya wasichana ya huruma inayomilikiwa na shirika la watawa wakatoliki la misericodia iliyopo jimbo katoliki mjini Dodoma ambapo mahafali hayo yalikwenda sambamba na jubilei ya miaka 50 tangu watawa hao wa misericodia kuanza kutoa huduma za elimu hapa nchini.

Dr. Nchimbi aliongeza kuwa katika ulimwengu wa sasa wa utandawazi na maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano kumekuwa na maumizi mabaya ya teknolojia hizo yanayofanywa na wanafunzi matokeo yake tunazalisha wataalamu na viongozi wasiokuwa na maadili  na pia amezitaka shule ningine hapa nchini kujipanga nazo kupambana na tatizo hili.

Mkuu huyo wa mkoa pia alishukuru mchango mkubwa unaotolewa na taasisi za dini katika kuhudumia jamii akiainisha upande wa kutoa huduma za elimu kwa jamiinna kusema kuwa serikali inatambua na kuthamini sana mchango huo na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa taasisi hizo za kidini ili kwa pamoja waendelee kuhudumia jamii na kusaidia kuleta maendeleo hapa nchini.

Kwa upande wake askofu mn'gatuka wa jimbo katoliki Dodoma Mwashamu Martias Isuja akitoa historia alisema kuwa miaka ya hapo awali mfumo wa elimu hapa nchini ulikuwa finyu hasa kwa upande wa wasichana kwenda shule ndipo kanisa kupitia mashirika yake mbalimbali yakaanza kuwekeza kwenye elimu. Aliielezea shule hiyo ya Huruma kama miongoni mwa shule za kwanza hapa nchini ambazo zilianza kwa kutoa huduma za stadi/maarifa ya nyumbani na kuendelea kupiga hatua mpaka leo hii.

Kwa upande wao wahitimu wa kidato cha nne wakiwakilishwa na mwanafunzi Ritah George aliyesoma taarifa ya wanafunzi wanaotarajiwa kuhitimisha masomo yao ya kidato cha nne mwaka huu wameomba uongozi wa shule kushughulikia changamoto za maktaba yenye nafasi za kutosha, vifaa vya kujifunzia kama kompyuta,viwanja vya michezo na walimu wa michezo.




Sehemu ya wanafunzi 46 wanaotarajia kuhitimu kidato cha nne katika shule ya sekondari ya wasichana ya Huruma iliyoko mjini Dodoma wakisikiliza salamu za mkuu wa Mkoa wa Dodoma (hayupo pichani) wakai wa mahafali ya 9 ya kidato cha nne shuleni hapo yaliyoenda sambamba na jubilei ya miaka 50 tangu watawa wa misericordia kuanza kutoa huduma za elimu hapa nchini, mahafali hayo yalifanyika mwishoni mwa wiki.

No comments:

Post a Comment