Saturday, December 7, 2013

JUMLA YA MAKOSA 2425 YANAYOHUSU UKATILI WA KIJINSIA YARIPOTIWA DODOMA.


Na John Banda, Dodoma
DAWATI la kupinga ukatili wa kijinsia na watoto lililopo katika mpango
wa polisi jamii limetangaza jumla ya makosa 2425 yanayohusiana na
vitendo vya ukatili wa kijinsia kuwandiyo yaliyoripotiwa polisi mkoani
Dodoma kati ya Januari 2009 mpaka octoba mwaka huu.

Hayo yalisemwa na mkuu wa Dawati hilo [ASP] Hamida Hiki wakati wa
 madahalo wa maadhimisho ya siku 16 za kupinga
ukatili wa kijinsia kanda ya kati.

Alisema  makosa ya ukatili wa kipigo yalikuwa 1020, yakifuatiwa na ubakaji
794, shambulio 411, Ulawiti 179 kutupa watoto 14 ma matukio saba  ya wizi
wa watoto.

Alizitaja  changamoto katika kukabiliana na vitendo vya ukatili wa kijinsia
ni jamii bado ina mfumo dume hivyo kuwa chanzo cha ukatili, kuendelea
kuwepo kwa mila potofu kama ukeketaji na kuozesha mabinti wakiwa na umri
mdogo, kuongezeka kwa wimbi la watoto wa mitaani, ulevi wa kupindukia na
matumizi ya madawa ya kulevya.

Pia hali duni ya uchumi inayopelekea kushamiri kwa biashara ya binadamu
hasa kwa wasichana kupelekwa mijini  kutafuta ajira na mashahidi kushindwa
kujitokeza kwa wakati kwa ajili ya kutoa ushahidi mahakamani.

Alisema tangu kuanzishwa kwa dawati la jinsia miongoni mwa mafanikio
yaliyopatikana ni ongezeko la kesi za unyanyasaji wa kijinsia kuripotiwa
tofauti na awali waathirika walikuwa hawatoi taarifa kwenye vituo vya
polisi.

Pia jamii kuwa na imani na Jeshi la Polisi hivyo ushirikiano na mahusiano
katika suala la kupinga vitendo vya ukatili umeongezeka, kuboreshwa kwa
huduma za jinsi na kushughulikia makosa ya jinsia na watoto ambapo huduma
hizo sasa zipo hadi ngazi ya vituo vidogo.

Nae Mkurugenzi wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali linalopinga ukatili dhidi ya
wanawake na watoto (AFNET) Sarah Mwaga anaitaka jamii kutoa ushirikiano ili
vitendo vinavyohusiana na ukatili wa kijinsia vikomeshwe.

Mdahalo huo uliandaliwa na Mtandao wa Kupambana na Ukatili wa kijinsia
(MKUKI) ulioratibiwa na AFNET kwa kushirikiana na Shirika la Wanawake katika
Sheria na Maendeleo Barani Afrika (WILDAF) Tanzania na Jeshi la Polisi Mkoa
wa Dodoma.

Mwisho

No comments:

Post a Comment