Thursday, May 1, 2014

SHEREHE ZA MEI MOSI ZAINGIA DOSARI MFANYAKAZI WA IKULU AFIA UWANJANI JIJINI DAR ES SALAAM

  
 Baadhi ya jamaa aliyoambatana nao wakimwangalia mara baada ya kufikishwa chumba cha huduma ya kwanza.
MAADHIMISHO ya Siku ya Wafanyakazi Kitaifa, maarufu kama Mei Mosi yaliyofanyika leo jijini Dar es Salaam yameingia dosari baada ya mmoja wa wafanyakazi kufariki dunia uwanjani kwa ghafla akiwa katika maadhimisho hayo.


Mfanyakazi huyo anayedaiwa kufanyakazi Ikulu alizidiwa ghafla akiwa katika maandamano na kupatiwa huduma za kwanza lakini hali yake ilizidi kuwa mbaya na hatimaye kudaiwa kupoteza maisha akipatiwa huduma na madaktari na wahudumu kutoka kikosi cha msalaba mwekundu waliyokuwa katika maadhimisho hayo.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia mfanyakazi huyo akiletwa katika kambi ya watu wa huduma ya kwanza iliyokuwa katikati ya uwanja wa Uhuru, kisha kupatiwa huduma ya kwanza bila mafanikio na baadaye alifariki dunia.

 Kwa mujibu wa taarifa kutoka katika kundi ambalo lilimleta mfanyakazi huyo baada ya kuzidiwa ghafla lilimtaja kuwa jina lake ni Rashid John Chilwangwa.

Mmoja wa wafanyakazi waliokuwa wameandamana na mfanyakazi huyo ambaye hakupenda kutaja jina lake kwa kuwa yeye si msemaji akisimulia tukio hilo, alisema John Chilwangwa (45) walikuwa naye katika sherehe za maadhimisho na hali yake ilibadilika kabla ya kuingia uwanjani na aliomba aende kujisaidia haja ndogo baada ya hapo alianza kuishiwa nguvu.

“…Si tulishangaa alikaa muda kidogo akijisaidia baada ya kumfuata tulimkuta ametoka ndani ya choo na kuja nje na kisha kukaa kwenye tofali huku akisema anajisikia kuishiwa nguvu na hali ilibadilika ndo tukamleta hapa,” alisema shuhuda huyo.

Alipoulizwa hali yake kwa sasa ambapo alikuwa ameingizwa kwenye hema la huduma ya kwanza kwa wahudumu kutoka kikosi cha msalaba na madaktari alisema wamejaribu kumuhudumia lakini bahati mbaya amefariki dunia tayari.
“…Tumeambiwa na madaktari kuwa ameshafariki tayari,” alisema shuhuda huyo ambaye alikuja na mgonjwa huyo.

Mwandishi wa habari hizi alishuhudia madaktari wakijaribu kumtundikia dripu huku wakijaribu kurudisha mapigo ya moyo kwa kushtua mara kadhaa lakini juhudi ambazo hazikuzaa matunda. 

Baada ya kubaini amefariki dunia walisita kumwekea dripu ambayo ilikuwa inaandaliwa na badaye walimfunika kwa shuka nyeupe na kuita gari la wagonjwa tayari kwa kumpeleka hospitali kwa uchunguzi zaidi. 

Hata hivyo hakupatikana mara moja daktari kuzungumzia kilichomsibu Chilwangwa

No comments:

Post a Comment