Tuesday, May 6, 2014

BOMU LALIPUKA KATIKA KANISA LA KKKT JIJINI MWANZA NA KUJERUHI WAUMINI.


Picha ya kanisa kutoka maktaba/ Picha kamili kuwajia hivi punde.
MHUDUMU wa nyumba ya kupumzikia wageni wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Mashariki ya Ziwa Victoria, jijijini hapa, amejeruhiwa vibaya baada ya kulipukiwa na bomu lililokuwa limewekwa kwenye korido la nyumba hiyo.

Tukio hilo lilitokea jana (Jumatatu), kati ya saa 1:45 na saa 2:20 usiku, katika eneo la Makongoro wilayani Ilemela wakati mhudumu huyo Bernadetha  Alfred (25) alipofungua kifurushi cha mzigo alichodhani kimesahaulika kwenye eneo hilo, kabla ya kumlipukia.

Kwa mujibu wa Katibu wa Dayosisi hiyo, Mollel Rogart, kifurushi hicho kilichokuwa kwenye mfuko mweusi wa nailoni, kilikuwa juu ya kreti (tupu) za soda, karibu na eneo la kulia chakula lililopo katika nyumba hiyo.

“Ule mfuko ulikaa pale siku tatu ndiyo usiku huo mhudumu wetu akakichukua kukiangalia akidhani ni mzigo wa mtu umesahaulika.” Alieleza Katibu huyo na kudai kuwa kifurushi hicho kilimlipukia mara tu alipokifungua na kujeruhi vibaya katika sehemu mbalimbali za mwili.

Kamanda wa polisi mkoani Mwanza, Valentino Mlowola akithibitisha tukio hilo, alisema kwamba uchunguzi wa awali uliofanywa na kikosi maalum kutoka Dar es salaam umebaini kuwa bomu hilo limetengenezwa kienyeji.

Mlowola alieleza kuwa, Bernadetha aliyejeruhiwa vibaya katika sehemu mbalimbali za mwili, alikimbizwa katika Hospitali ya rufaa ya Bugando ambako anaendelea na matibabu.

Kamanda  huyo alieleza kwamba, mabomu (yakiwemo ya kienyeji) yako katika mifumo mbalimbali hivyo wananchi hususan wahudumu wa sehemu za mikusanyiko wawe na tahadhari na vitu vinavyoonekana kusahaulika na wasisite kuwajulisha polisi vinapoonekana hivyo. 

Mlipuko huo uliozusha hofu kwa waumini mbalimbali wakiwemo wa Kanisa hilo, umetokea ikiwa ni wiki moja baada ya maadhimisho ya ‘Huduma ya Mtoto’ kwa makanisa mbalimbali ya Kikristu jijini hapa yaliyofanyika kwenye kanisa hilo, yakitanguliwa na maandamano kutoka uwanja wa furahisha hadi KKKT.

No comments:

Post a Comment