Saturday, May 17, 2014

MAAJABU ! NJAA YASABABISHA FAMILIA KULA NYAMA YA PAKA.


Siyo rahisi kwa mtu ambaye anapata chakula kutwa mara tatu, kuamini kuwa kuna binadamu ambao wanaweza kuishi hata siku tatu bila kupata hata mlo mmoja.
Hata hivyo ni ukweli usiopingika kuwa wakati unakula na kumwaga chakula kwenye mifuko ya takataka, wapo ambao hutamani kukimbilia mifuko hiyo na kujitafutia chochote kwa ajili ya matumbo yao.(Martha Magessa)
Wapo ambao hudiriki kula hata vitu ambavyo havistahili kuliwa na binadamu, lakini hawana jinsi wanafanya hivyo kutuliza matumbo yao yanayosumbuliwa na njaa.
Njaa imekuwa ni tatizo sugu linaloonekana kujitokeza katika mataifa mbalimbali yanayoendelea, huku bara la Afrika likiwa limeathirika kwa sehemu kubwa kutokana na janga hili.
Licha ya kuwa na eneo kubwa la ardhi yenye rutuba na mvua za kutosha, ukanda wa Afrika Mashariki nao umekuwa ukikumbwa na baa hili katika baadhi ya maeneo.
Hilo linatokana na maeneo hayo kuwa na ukame na kukosa mvua, hali inayopelekea kilimo kutofanyika kama inavyostahili hivyo chakula kuwa miongoni mwa vitu hadimu kupatika kwa wakazi wa eneo husika.
Kijiji cha Kakoghit kilichopo kwenye Kata ya Lokis nchini Kenya, kimekuwa miongoni mwa maeneo ambayo yapo katika hali mbaya zaidi kutokana na tatizo la njaa.
Tukio la hivi karibu la familia moja kuchinja paka na kumla kama kitoweo baada ya kuzidiwa na njaa waliyokaa nayo kwa siku kadhaa kutokana na kukosa chakula, limedhihirisha namna gani njaa ilivyokuwa tishio.
Familia hiyo yenye jumla ya watu watatu ikiwajumuisha Jepoterit Yaranyang (80), Jepteker Ng'uriawing (35) na mtoto wake wa miaka miwili ilifikia uamuzi wa kumuiba paka wa jirani na kumchinja ili kutuliza njaa iliyokuwa ikiwasumbua kwa muda mrefu.
Katika mahojiano yake na gazeti la moja nchini Kenya, Ng'uriawing anasema kuwa baada ya kukaa siku nyingi bila kula huku mama yake akiwa hoi kitandani akidhoofika kutokana na njaa, akafikiria kumkamata paka wa jirani ili wamfanye kitoweo. Wazo hilo likatawala kichwani mwake na dakika chache alipokatiza paka huyo alimpiga kichwani kabla ya kumchinja na kuchoma nyama yake kuitafuna ili kupoza njaa iliyokuwa ikiwakabili.
"Baada ya kuona hali inazidi kuwa mbaya nikaona tutaangamia kwa kuwa mama yangu tayari alishaanza kudhoofika kutoka na njaa, nikaamua kumgonga paka kisha nikamchuna ngozi na kuchoma nyama yake ambayo ilikuwa na damu nyingi"anasema Ng'uriawing na kuongeza:
"Ukweli ni kwamba hali ilikuwa mbaya sana hata kama paka asingejitokeza ingewezekana ningemchinja mtoto wangu tuile nyama yake maana nisingeweza kuvumilia hali ya njaa kali kiasi kile"

No comments:

Post a Comment