Thursday, January 2, 2014

MAMA MZAZI WA IGP ERNEST MANGU AMTAKA MTOTO WAKE KUFANYA KAZI KWA UADILIFU.


mama 0053e
Mama Mzazi wa Mkuu wa Polisi nchini (IGP), Ernest Mangu, Mwanaidi Msengi, amemsihi mwanawe kufanya kazi kwa bidii asimwangushe Rais Jakaya Kikwete ili asije kujutia kumpa nafasi hiyo.
Mwanaidi alisema licha ya furaha kubwa aliyonayo, anamuasa mtoto wake kuchapa kazi kwa bidii kama njia mojawapo ya shukurani kwa Rais Kikwete kwa kumteua akiwa mwenyeji wa kwanza kutoka Mkoa wa Singida kushika wadhifa huo nyeti.(HD)
"Hii ni heshima kubwa sana kwangu binafsi, ndugu zake, wakazi wa Kijiji cha Kihunadi na Mkoa wa Singida, kwa hiyo lengo langu ni kumwombea mtoto wangu Mangu asimwangushe Rais... Eee Baba (Mungu) msaidie mwanangu atimize wajibu wake ipasavyo ili Rais Kikwete siku moja aseme hakukosea kumpa Mangu ukuu wa polisi," alisema Mwanaidi.
Juzi ndugu, jamaa na marafiki walifanya hafla ndogo iliyoambatana na vifijo, nderemo na bashasha na wakazi wa Kijiji cha Kihunadi, Tarafa ya Ilongero, mkoani Singida, alikozaliwa IGP huyo huku wakidai sasa kijiji chao kitajulikana haraka ndani na nje ya Tanzania.
Walisema licha ya kujulikana, changamoto mbalimbali zinazokikabili kijiji hicho zitapatiwa ufumbuzi wa kudumu mapema iwezekanavyo.
Mwanaidi alisema Mangu alianza kumwonyesha mafanikio tangu Shule ya Msingi Kinyagigi, kwani alikuwa na bidii ya kujisomea mara kwa mara alishika nafasi ya kwanza au ya pili.
Kwa mujibu wa Mwanaidi, IGP Mangu ni mtoto wa pili kati ya saba aliowazaa.
"Mangu ni wa pili kati ya watoto wangu saba baada ya kuolewa na baba yao, Jumbe Omari Mangu aliyefariki Aprili 27, 1988. Jina la Jumbe linatokana na kupewa kazi ya ujumbe wa wakoloni wakati wa ujana wake," alisema.
Wenyeji wa kijiji hicho, walisema wamekuwa wakiamini Mangu atafika mbali kwa kushika nafasi za juu za uongozi, kutokana na uadilifu, uchapaji kazi, ukaribu wake na wananchi, uaminifu na uwazi.
Mwanaidi alisema Mangu alipofaulu kwenda sekondari alilazimika kuomba ng'ombe kwa mke mweza, ili akamuuze apate fedha za kugharimia masomo ya mtoto wake.
"Mke mwenzangu alimtoa ng'ombe wake, lakini Mangu alipomuuza kwenye mnada pale Singida mjini, aliibiwa fedha zote na alirudi nyumbani akilia sana," alisema.
Alisema baada ya hapo alimwambia mtoto wake kwamba, ataanza kutengeneza vyungu kwa kutumia udongo wa mfinyanzi ili kupata fedha za kugharimia masomo yake."Nashukuru Mangu alinielewa vizuri kwa sababu alishiriki kubeba kichwani vyungu hivyo wakati wa kuviuza hadi kichwa chake kilikaribia kuwa kipara. Nilibuni chanzo kingine cha mapato ambacho kilikuwa ni kukoroga na kuuza pombe za kienyeji," alisema. Inadaiwa baba yake, IGP Mangu alioa wanawake sita kwa nyakati tofauti, lengo likiwa ni kupata mtoto wa kiume. Wengi wa wake zake walikuwa wakizaa watoto wa kike.

No comments:

Post a Comment