Saturday, January 4, 2014

CHADEMA KWAWAKA MOTO WANACHAMA WACHAPANA MAKONDE MAHAKAMANI.

adema dceb7
Vurugu za aina yake zimezuka katika Mahakama Kuu jijini Dar es Salaam, baada ya watu wanaodhaniwa kuwa wanachama wa Chadema kumzomea aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama hicho, Zitto Kabwe.
Vurugu hizo zilihusisha wafuasi wa chama hicho wanaomuunga mkono Zitto na wale wanaompinga, ambao walikuwa wamebeba mabango ya kumsifia na wengine wakiwa wamebeba ya kumkashifu.
Katika vurugu hizo, baadhi ya wanachama hao waliamua kufanya doria isiyo rasmi ndani ya mahakama hiyo ya kuwasaka watu waliodai kuwa ni mamluki, huku wakimkamata askari kanzu, kabla ya kumpiga ngumi na kumchania shati mtu mmoja wakidai kuwa alikuwa akiwarekodi kwa kutumia simu yake ya mkononi.
Tukio hilo la aina yake lilitokea jana asubuhi ambapo kundi la wanachama hao, huku baadhi wakiwa wamevaa nguo za kaki zinazotumiwa na chama hicho kufika katika mahakama hiyo kwa lengo la kusikiliza kesi ya pingamizi iliyofunguliwa na Zitto.
Mara baada ya kuwasili kwa Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini, huku akiwa ameongozana watu kadhaa wakiwamo wanasheria wake na mabaunsa, wanachama hao walianza kumzomea huku baadhi wakimwita fisadi.
Hali hiyo iliibua zogo katika eneo la mahakama hiyo, hali iliyowalazimu maofisa kadhaa wa polisi kuingilia kati kwa kuamua kumchukua Zitto na kumhifadhi kwenye chumba maalumu na kumtoa saa 6 mchana kesi yake ilipoanza kusikilizwa. Baadhi ya mabango ya kumkashifu yalisomeka; Zitto tulimpenda, CCM imempenda zaidi, Zitto rudisha fedha za CCM.
Yale yaliyomsifia yalisomeka; Zitto kama Mandela na Zitto ni Mkombozi.Baada ya kumalizika kusikilizwa kwa kesi hiyo, saa 12 jioni wanachama hao walianza kurushiana ngumi, hasa baada ya kuibuliwa kwa mabango yaliyosomeka 'Zitto kwanza Chadema baadaye'.
Awali hali hiyo ilimfanya Zitto kutaharuki, huku mabaunsa wake wakijihami na kuanza kumlinda.
Baada ya Zitto kuhifadhiwa baadhi ya wanachama hao ambao waliingia kwa kuandikishwa majina yao getini, walianza kuwasaka watu waliowahisi kuwa mamluki, ambapo walimnasa askari kanzu na kuanza kumzonga wakimuhoji anapeleleza nini katika eneo hilo.
"Hapa tunataka kujua wewe ni nani na unataka nini hapa, maana hatukuelewi kabisa kwa nini unakuja kusikiliza mazungumzo yetu, jitambulishe," alisisika mmoja wa wanachama hao akimhoji askari huyo huku akiwa amemkandamiza ukutani,
"Tunajua wewe ni askari kwa nini hujavaa sare leo? Kisha unajichanganya kwenye kundi letu."
Kesi hiyo ilimalizika saa 12 jioni ambapo Zitto alitolewa chini ya ulinzi mkali wa polisi kwa kupitia mlango wa nyuma wa mahakama hiyo na kuwaacha wafuasi hao wakionyeshana ubabKabla ya kuanza kwa kesi hiyo, Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Tundu Lissu alimwomba Jaji John Utamwa kuendesha kesi hiyo kwa lugha ya Kiswahili kwa kuwa inagusa sehemu ya masilahi ya umma, jambo ambalo liliibua shangwe kwa wafuasi wa chama hicho waliokuwa wamefurika katika mahakama hiyo.
Hata hivyo baada ya kesi kuanza kuendeshwa kwa lugha ya Kiswahili, Jaji Utamwa alilazimika kuikatiza, na kuwakemea wanachama wa Chadema baada ya sauti za kuguna kusikika wakati wakili wa Zitto, Albert Msando alipokuwa akiwasilisha hoja kuhusu msingi wa kesi hiyo.
" Nataka kuwakumbusha hapa mahakamani ni tofauti na sehemu nyingine sauti zinazosikika sizitaki, anayeona kwamba yanayozungumzwa hakubaliani nayo kama hawezi kunyamaza atoke nje vinginevyo hatua za kisheria zitachukuliwa," alisema Jaji Utamwa.
Kundi la Wanachadema hao huku wengine wakiwa wamevalia sare zao waliwasili mahakamani hapo ili kusikiliza kesi ya pingamizi iliyofunguliwa na Kabwe akiiomba Mahakama iwazuie Bodi ya Wadhamini wa Chadema, Katibu Mkuu pamoja na Kamati Kuu ya Chadema jana kumjadili, kumchukulia hatua, uamuzi wowote wala kuhusu uanachama wake.
Msingi wa kesi
Juzi Zitto aliomba Mahakama hiyo kuzuia Kikao cha Kamati Kuu ya Chadema kumjadili hadi rufaa yake aliyoikata kwenye Baraza Kuu la Chadema itakaposikilizwa na kuamuliwa na wazuiwe kumwingilia katika utekelezaji wa majukumu yake ya ubunge wa Kigoma Kaskazini .
Pia aliiomba Mahakama hiyo Kuu kumwamuru Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Wilbroad Slaa ampatie nakala ya mashtaka na maelezo ya uamuzi uliofikiwa na Kamati Kuu Novemba 22, 2013 na kusababisha avuliwe nyadhifa zake ili aweze kupeleka rufaa yake Baraza Kuu la Chadema kupinga uamuzi huo

No comments:

Post a Comment