Monday, June 17, 2013

KUFUATIA MLIPUKO WA BOMU ARUSHA WABUNGE CHADEMA WAGOMA KUINGIA BUNGENI.


Wakati Jeshi la Polisi nchini limesema limepata taarifa za mwonekano wa mtu aliyetupa bomu katika mkutano wa kampeni wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Arusha, Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe amesema wabunge wake leo hawataingia bungeni.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mbowe alisema wabunge hao watawasili Arusha kwa ajili ya kuungana na wananchi pamoja na wanachama kwenye msiba huo.
Alisisitiza kwamba kuanzia leo mahema yatawekwa viwanja vya Soweto kwa ajili ya kuomboleza msiba huo na mara polisi wakimaliza uchunguzi wao na kutoa majibu juu ya vifo hivyo, marehemu hao watasafirishwa.
Wakati Mbowe anatoa kauli hiyo Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi akizungumza jana mjini Arusha na waandishi wa habari, alisema taarifa za awali zinaonesha mlipuko huo ni bomu la kutupwa kwa mkono (grumeti) na hivi sasa timu ya wataalamu ikiongozwa na Kamishna wa Operesheni Maalumu wa Jeshi la Polisi, Paul Chagonja inaendelea na uchunguzi wa tukio hilo.
Naye Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Said Mwema katika taarifa yake kwa vyombo vya habari ameahidi kupambana na kuhakikisha wahusika wanapatikana.
Alitoa taarifa hiyo jana kwa waandishi wa habari Dar es Salaam na kusema hadi jana, watu waliothibitika kufa katika tukio hilo ni wawili na 68 ni majeruhi.
Waliokufa ni Katibu wa Baraza la Wanawake (Bawacha) wa Chadema, Kata ya Sokoni 1, Judith Moshi (25) na mtoto aliyejulikana kwa jina moja la Justin.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

No comments:

Post a Comment