Kamati
Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa imejadili na kutolea maamuzi pamoja na
mambo mengine suala la Madiwani wanane waliotangazwa kufukuzwa uanachama
na Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera.
Katika
maamuzi yake, Kamati Kuu imebatilisha uamuzi uliofanywa na Halmashauri
Kuu CCM ya Mkoa wa Kagera Agosti 13, 2013 wa kuwafukuza uanachama
Madiwani hao. Hivyo Madiwani hao wanane ni wanachama halali wa CCM.
Kamati Kuu imetoa uamuzi huo,
baada ya kubaini kuwa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Kagera
haikuzingatia Katiba ya CCM ya 1977 Toleo la 2012 Ibara ya 93 (15).
Ibara hiyo inasomeka kuwa moja ya kazi ya Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa
ni:-
“Kumwachisha au kumfukuza
uongozi kiongozi yeyote ambaye uteuzi wake wa mwisho unafanywa na
Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa, isipokuwa kwa suala la kumvua uanachama
au uongozi Diwani lisifanyike hadi Kamati Kuu imearifiwa na kutoa
maelekezo”.
Aidha, Kamati Kuu imewaonya
Madiwani wa CCM wa Manispaa ya Bukoba, Mbunge wa Bukoba Mjini na Meya
kwa kusababisha kukosekana kwa utulivu, mshikamano na amani katika
Manispaa na Chama.
Kamati Kuu pia imeitaka
Serikali kumwagiza mdhibiti na mkaguzi mkuu wa serikali(CAG) kufanya
ukaguzi maalum wa haraka wa mambo yanayolalamikiwa dhidi ya Meya ili
ukweli ujulikane na matokeo ya uchunguzi huo yasilishwe kwenye baraza la
madiwani ili hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria na taratibu
zinazoongoza Serikali za Mitaa.
Wakati tuhuma hizo dhidi ya
Meya zikichunguzwa; Kamati Kuu inawataka Madiwani wa CCM kurejesha
utulivu kwenye Manispaa na Chama kwa ujumla ili kufanikisha utekelezaji
wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM na kuwaletea maendeleo wananchi wa Bukoba.
No comments:
Post a Comment