Monday, July 15, 2013

CHADEMA WANG'ARA WAIGALAGAZA CCM 4 BILA ARUSHA.



wafuasi wa chadema wakiwa katika moja ya mikutano yao.
ARUSHA. Chadema kimethibitisha umwamba wake katika siasa za Jimbo la Arusha Mjini, baada ya kutetea kwa kishindo kata zake nne kwenye uchaguzi mdogo wa udiwani uliofanyika jana.
Katika uchaguzi huo uliokuwa unasubiriwa kwa hamu na ambao ulichukuliwa kama kipimo cha siasa za Arusha ambazo zimekuwa na mvutano mkubwa, Chadema kiliongoza katikia vituo vyote 136 vya kupigia kura Kata za Elerai, Kaloleni, Kimandolu na Themi.
Kata hizo zilikuwa wazi tangu mwaka 2011 baada ya Chadema kuwatimua wanachama wake waliokuwa madiwani Estomih Mallah(Kimandolu), John Bayo (Elerai), Reuben Ngowi (Themi) na Charles Mpanda (Kaloleni).
Matokeo
Katika matokeo yaliyotangazwa na Msimamizi wa Uchaguzi Kata ya Elerai, Obedi Meng’oriki mshindi alikuwa Jeremiah Mpinga wa Chadema aliyepata kura 2,047 dhidi ya 1,471 za Emmanuel Laizer wa CCM. Katika Kata hiyo kulikuwa na wagombea wengine ambao ni John Bayo (CUF; kura 302), Seif Shimba (CCK; kura 3) na Boisafi Shirima (TLP;1).
Katika Kata ya Themi, Kinabo Edmund wa Chadema aliibuka na ushindi baada ya kupata kura kupata kura 674. Msimamizi wa Uchaguzi Kata hiyo, Ezeka Mboya alisema Kinabo alifuatiwa na Victor Mkolwe aliyepata kura 326 na Lobora Ndarpoi wa CUF alipata kura 307.
Kata ya Kaloleni, Msimamizi wa Uchaguzi, Anna Ledisa alimtangaza Kessi Lewi wa Chadema kuwa mshindi kwa kura 1,470 dhidi ya Emmanuel Mliari wa CCM aliyepata kura 330 na Abbas Mkindi wa CUF aliyepata kura 275 na Ngilishi Pauli wa Demokrasia Makini aliyeambulia kura mbili.
Kata ya Kimandolu, Msimamizi wa Uchaguzi, Suleiman Kilingo alimtangaza Mchungaji Rayson Ngowi wa Chadema kuwa mshindi kwa kura 2,761 na kumshinda Edna Saul wa CCM aliyepata kura 1,163. Kwa matokeo hayo, Chadema sasa kimefikisha madiwani 12 wakati CCM kimebakiwa na kumi na moja na TLP kina wawili.
Ushindi huo wa Chadema una athari kwa nafasi ya Meya wa Jiji la Arusha, Gaudence Lyimo kwani CCM kina wajumbe 14 tu kwenye Baraza la Madiwani, TLP wawili wakati Chadema sasa kimefikisha 15. Wabunge wa majimbo na wale wa viti maalumu pia ni madiwani.
Aidha, Chadema kina nafasi ya kuongeza kiti kingine cha udiwani kwani Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kinatarajiwa kuitisha uchaguzi mdogo Kata ya Sombetini.
Mkurugenzi wa NEC, Julius Malaba alimwambia mwandishi wetu kuwa tume yake inatarajia kuitisha uchaguzi mdogo hivi karibuni baada ya kata hiyo kutangazwa wazi na Ofisi ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tamisemi.
Malaba alisema uchaguzi huo utaitishwa baada ya aliyekuwa Diwani wake, Alphonce Mawazo kujitoa CCM na kujiunga na Chadema hali inayokifanya chama tawala kuwa katika wakati mgumu kukitetea kiti hicho.

No comments:

Post a Comment