Askari saba wa kikosi cha kulinda amani cha
Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika wameuawa katika shambulizi la kuvizia huko
Darfur, magharibi mwa Sudan.
Tukio hilo la Jumamosi limetajwa kuwa baya
zaidi katika historia ya miaka mitano ya kikosi hicho cha Umoja wa Mataifa na
Umoja wa Afrika kijulikanacho kama UNAMID.
Kaimu Msemaji wa UNAMID Christopher Cycmanic
amesema hujuma hiyo ilIjiri katika kituo cha walinda amani cha Manawashi
kaskazini mwa Nyala mji mkuu wa jimbo la Darfur Kusini. Ameongeza kuwa askari
wa UNAMID walishambuliwa na kundi la watu wenye silaha ambao hawakuweza
kutambulika wakati huo.
UNAMID haijatangaza uraia wa maafisa
waliouawa lakini wanaosimamia amani katika eneo hilo ni askari kutoka Tanzania.
Kati ya waliopoteza maisha ni wanawake wawili wanaohudumu kama polisi wa
kulinda amani.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban ki-Moon
amelaani vikali shambulizi hilo dhidi ya UNAMID.
Ametoa wito kwa serikali ya Sudan kuchukua
hatua za haraka kuwakamata na kuwachukulia hatua za kisheria wahusika. Mji wa
Nyala ambao ndio mkubwa zaidi katika eneo la Darfur umekumbwa na tatizo la
ukosefu wa usalama katika siku za hivi karibuni.
No comments:
Post a Comment