Katibu wa halmashauri kuu ya CCM (NEC) Itikadi, Siasa na Uenezi akiwahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika mjini Kahama
- Adai ndio chanzo cha kupigana bungeni
- Asema ndizo walizotumia kuzunguka na helkopta nchini.
- Aeleza yaliyotokea bungeni sio bahati mbaya, Chadema waliyapanga
- Ashukuru bunge kuendelea kuonyeshwa"live" ili wananchi waone ujinga wao.
- Awatuhumu kuweka masilahi yao mbele badala ya nchi.
- Asisitiza CCM kuendelea kuheshimu uamuzi wa wananchi juu ya katiba.
- Aonyesha madai ya Chadema kitakwimu yasivyojali wakulima na wafanyakazi.
Katibu wa NEC ya CCM itikadi na Uenezi amesema
kinachowasumbua Chadema mpaka wanafanya yote waliyoyafanya hasa ngumi na vurugu
bungeni ni namna watakavyoeleza kwa waliowapa pesa za kuvuruga mchakato wa
katiba nchini kwani wanatakiwa kupeleka mrejesho jinsi walivyofanikiwa na jinsi
walivyotumia mabilioni hayo.
Nape ameyasema hayo kwenye mkutano mkubwa wa hadhara mjini
Kahama kwenye ziara ya karibu siku ishirini kanda ya ziwa kwa mikoa mitatu
yaani Shinyanga,Simiyu na Mara ya Katibu Mkuu wa CCM Taifa Ndg. Abralhaman
Kinana.
"Wenzetu hawa nasikia wamepewa mabilioni toka nje kwa
kisingizio cha kushiriki mchakato wa katiba, na kama ilivyo kwa vibaraka
wengine katika bara la Afrika lengo la mapesa hayo sio kuwawezesha kushiriki
bali kuanzisha fujo na vurugu ili mchakato usimalizike salama iwe ajenda 2015
kwani kimsingi hawana ajenda mpya" alisisitiza Nape.
Akielezea swala la pesa kutoka nje Nape alisema mara tu
baada ya rasimu ya kwanza kutoka Katibu Mkuu wa Chadema alikwenda nje ya nchi
na akakaa kwa muda na aliporudi tu, ndio Chadema wakapanga kuanza kuzunguka na
helkopta.
"Babu atwambie alifuata nini nje? Na pesa za kuzunguka
na misafara miwili tofauti ya helkopta walitoa wapi? Na watwambie kama
walisharudisha mrejesho kwa wafadhili wao" alisema Nape
Nape aliendelea kusisitiza kuwa yote yaliyotokea bungeni si
mambo yaliyotokea kwa bahati mbaya isipokuwa ni mambo yaliyopangwa na Chadema
katika mkakati wa kutimiza moja ya malengo yao.Alisema ilikua ni lazima
watafute mahali pa kufanya kituko bungeni ili iwe mjadala na ili wapate sababu
na picha za kuonyesha kwa waliowapa pesa kuwa wanapambana.
"hili walilofanya Chadema bungeni ni jambo walilopanga
katika mkakati wao wa 'civil disobidiency' ...machafuko ya umma dhidi ya dola,
mkakati ambao unaratibiwa kutoka nje na baadhi ya wale waliokuwa wakoloni
katika nchi zetu za Afrika. Lengo ni kusababisha machafuko na nchi
kutotawalika" alisema Nape.
Nape alisema ndio maana CCM ilisisitiza lazima bunge
liendelee kuonyeshwa na televisheni ili kuonyesha yanayoendelea bungeni
kuwawezesha wananchi kuona kinachofanywa na wawakilishi wao.
"bila shaka wananchi mmeona kilichotokea bungeni kwa
macho yenu, sina haja ya kuwaeleza. Mmeona wabunge wa upinzani
walichofanya,uchaguzi ujao tupunguze idadi ya vichaa bungeni ili kodi zetu
zitumike vizuri,kwani tuliwatuma wakajadili maendeleo yetu wao wamegeuza bunge
uwanja wa masumbwi.
Aidha Nape akifafanua hoja ya upinzani bungeni juu ya idadi
ya wabunge wa bunge maalum la katiba alisema upinzani hawana hoja ya msingi
bali wanasukumwa na ubinafsi na ulafi wa madaraka.
"Hoja iliyowafanya wapigane bungeni haina mashiko,
wanataka idadi iongezwe ya wabunge wa bunge la katiba kutoka 357 mpaka 792.
Hivi nani anabeba mzigo huu wa kuwalipa hawa wabunge kama sio mwananchi wa kawaida?
Halafu mnajiita watetezi wa wanyonge? Hamuoni aibu?" alihoji Nape.
Akiendelea kufafanua Nape anasema,
" katika hali ya kawaida tungetegemea wajenge hoja ya
kundi kubwa katika jamii ya kitanzania ambao ni wakulima na wafanyakazi ndio
wawe na uwakilishi mkubwa kwenye hilo bunge kama tunataka katiba kweli ya
wananchi lakini badala yake wao wanapendekeza wawakilishi kutoka vyama vya
siasa ukiacha wabunge waliopo sasa wawe 72 na wakulima wawe 10 tu! Wanataka
katiba ya vyama vya siasa badala ya katiba ya nchi kwa ajili ya wananchi.
Wanataka wafugaji wawe 10 tu na wafanyakazi 40. Kwa uwiano wa kawaida asilimia
80% wa wananchi wa nchi hii ni wakulima, tungetegemea wangependekeza idadi yao
kuwa kubwa lakini wao wanawapuuza wakulima na wafugaji kwa kudai wawe kumi
tu"!
Nape alimalizia kwa kudai kuwa siku za vyama kama Chadema
zinahesabika maana hii ya katiba ndio ilikuwa karata yao ya mwisho.
" Nimalizie kwa kuwatahadharisha vijivyama hivi vingine
kama CUF, NCCR mageuzi na wengine kuwa wenzao wamepewa mapesa wao wanwaunga
mkono kwa ajenda iliyojificha. Na kwakuwa hili la kuvuruga katiba ndio karata
yao ya mwisho basi tutarajie anguko baya sana kwa Chadema na huo ndio utakuwa
mwisho wao"!alimalizia Nape
No comments:
Post a Comment