Vita vya maneno kati ya Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, Zitto Kabwe imefika pabaya. Vita
hiyo ya maneno iliyoanzishwa na Lema katika kikao cha wabunge wiki
iliyopita kwamba Zitto anafanya unafiki kukataa posho, jana iliingia
katika hatua nyingine baada ya mwakilishi huyo wa Arusha kumshushia
tuhuma Mbunge huyo wa Kigoma Kaskazini kwamba anakataa posho za vikao
bungeni, lakini anapokea posho nyingi kutoka mashirika mbalimbali ya
kijamii nchini.
Lema
aliweka tuhuma hizo kwenye Mtandao wa Jamii Forum huku akisema kuwa,
suala hilo halihitaji vikao vya chama kulijadili isipokuwa vyombo vya
habari na hususani mitandao ya kijamii kwani hata Zitto hutumia mitandao
hiyo.
Katika hoja
yake, Lema alisema kuwa Zitto ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu
ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC) anakataa posho ya Sh70,000 kwa
kikao kimoja cha Bunge, lakini anapokea Sh700,000 mpaka Sh1,000,000 kwa
kikao kimoja cha kamati yake na haswa vile vinavyoandaliwa na mifuko ya
jamii.
Hata hivyo,
zitto alikanusha shutuma hizo akimtaka Lema kutoa ushahidi kama kuna
mjumbe yoyote wa kamati ya PAC anayepokea posho, huku akieleza kuwa
hawezi kubishana na Mbunge huyo wa Arusha mjini kwani yeye Zitto ni
kiongozi wake ndani ya Chadema.
“Naomba
kutaja masilahi yangu katika hili, wabunge wa kawaida wakialikwa katika
vikao hivyo huwa wanalipwa Sh500,000 kwa kikao kwa siku . Mimi nimewahi
kuhudhuria vikao hivyo mara mbili na nikalipwa hivyo pamoja na chai na
chakula cha mchana.” alisema Lema.
Lema alisema
posho hizo za wabunge ni tofauti na zile za Mwenyekiti wa PAC kwani
yeye pamoja na posho ya Sh700,000 mpaka Sh1,000,000 hupewa mafuta ya
gari au tiketi ya ndege ya kumtoa alipo na kumrudisha na kukodiwa hoteli
yenye hadhi ya nyota nne mpaka tano ambayo kwa siku gharama yake ni
Dola za Marekani 100 mpaka 600 kwa siku .
Akijibu hoja
hizo, Zitto alisema tangu siku nyingi alikwisha piga marufuku kwa PAC
kupokea posho kutoka taasisi au mashirika yanayosimamiwa na kamati hiyo.
“Toka
nimekuwa Mwenyekiti wa POAC (Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma) sio
tu nilipiga marufuku posho bali pia niliwashitaki PCCB (Taasisi ya
Kupambana na Kuzuia Rushwa) wabunge wanaochukua posho kutoka kwa taasisi
za Serikali,” alisema Zitto.
Alieleza
baada ya hatua hiyo, wabunge walihojiwa na PCCB kuhusu jambo hilo mpaka
aliyekuwa Spika wa Bunge wakati huo, Samuel Sitta alipoingilia kati na
kuwatetea wabunge hao.
“Hiyo
ilikuwa mwaka 2009 kabla hata Lema hajawa mbunge, wajumbe wa kamati ya
PAC wanalipwa posho za vikao kama wabunge wengine, lakini mimi sichukui
posho hizo za vikao,” alisema na kuongeza:.
“Sio tu PAC
hata kwenye Baraza la Madiwani na Baraza la Mashauriano la Mkoa wa
Kigoma na popote kule. Hata NGO (Mashirika yasiyo ya Kiserikali)
zikinialika kwenye vikao vyao sichukui posho za vikao. Nafasi yoyote
ninayoalikwa kama mbunge sichukui posho za vikao,” alisema Zitto.
Alisema mtu yeyote mwenye ushahidi wa yeye kuchukua posho za vikao popote pale auweke hadharani na atawajibika.
“Sio
kuandika uzushi au maneno ambayo mtu yeyote anaweza kuandika. Mimi
siwezi kubishana na Lema maana ni kiongozi wake katika chama. Natumaini
kadiri anavyokaa kwenye uwanja huu wa siasa atabadilika na kukomaa
zaidi,” alisema Zitto.
Kwenye hoja
yake, Lema alisema kuwa Chadema walikuwa wanakataa posho na kupendekeza
mishahara ipandishwe na posho zisizo za lazima ziondolewe ili kuondoa
mwanya wa ubadhirifu wa fedha za umma.
“Huu ndio uliokuwa msimamo wetu kulikuwa na msingi mkuu ambao ungekuwa na faida kubwa kwa nchi na watu wake,” alisema Lema.
Lema alisema
kwamba kabla msimamo huu haujawekwa hadharani na kutafsiriwa na Kambi
Rasmi ya Upinzani Bungeni, Zitto tayari alishatoka katika vyombo vya
habari na kujipambanua kuwa yeye hataki posho na wala hatachukua posho.
Lema alisema
kuwa, anaamini kuwa umaskini siyo uzalendo. “Sipendi umaskini, nachukia
umaskini, pia sipendi kuona mafanikio yangu yanabaki kwangu tu huku
wengine wakiteseka, lakini siwezi pia kukumbatia umaskini kwa lengo
lakuthibitisha uzalendo wangu.
Najua watu
wa jimbo langu wanataka maji , umeme na huduma bora za afya na mambo
mengi yenye sura hii, lakini sitang’oa bomba la maji nyumbani kwangu kwa
sababu jirani yangu hana maji ila nimtasaidia kwa kadiri nitakavyoweza
na yeye aepukane na adha hiyo ya ukosefu wa maji,” alisema Lema
No comments:
Post a Comment