TAARIFA YA ZITTO ZUBERI KABWE (MB) KUHUSU KUVULIWA NAFASI ZA UONGOZI NDANI YA CHAMA CHANGU CHA CHADEMA
1. Utangulizi:Katika kikao chake cha siku mbili kilichofanyika tarehe 20 - 22
Novemba 2013, Kamati Kuu ya CHADEMA, pamoja na mambo mengine, iliazimia
kunivua nafasi zangu zote za uongozi ndani ya chama. Kwa mujibu wa
taarifa ya chama iliyotolewa katika mkutano na waandishi wa habari siku
ya Ijumaa tarehe 22 Novemba 2013, ilielezwa kwamba sababu za kuvuliwa
uongozi mimi na Dk Kitila Mkumbo ni uhaini na hujuma kwa chama kutokana
na waraka unaojulikana kama mkakati wa uchaguzi 2013. Ukweli ni kwamba
waraka uliotajwa si sababu ya mimi kuvuliwa nafasi zangu za uongozi kama
ilivyojadiliwa katika Kikao cha Kamati Kuu . Sababu za kufukuzwa kwangu
kama zilizojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu ni tuhuma lukuki ambazo
si mara yangu ya kwanza kuzisikia zikijadiliwa ndani na nje ya vikao
vya chama. Hitimisho la tuhuma hizi ni kwamba mimi nimekuwa nikikisaliti
chama kwa kutumika na CCM na Usalama wa Taifa. Nitazianisha tuhuma hizi
na kuzijibu kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali
vyama.Ninatambua kwamba chama changu kinapita katika
wakati mgumu sana sasa hivi. Nataka nitamke mapema sana kwamba mimi
Zitto Zuberi Kabwe sitokuwa chanzo cha CHADEMA kuvunjika. Hiki ndicho
chama kilichonilea na kunifikisha hivi nilivyo. Ningependa chama hiki
mtoto wangu atakapokuwa mtu mzima na atakapoamua kujiunga na siasa
aingie CHADEMA. Bado nina imani kubwa na chama changu na ninaamini
ndicho kinachostahili kuendesha nchi jana, leo na kesho.
2. Kuhusu tuhuma mbalimbali zinazo elekezwa kwangu
Zipo tuhuma nyingi ambazo zimekuwa zikirudiwarudiwa katika vikao
vya chama na nje ya vikao na baadhi ya viongozi wenzangu. Tuhuma hizi
zinalenga kuonyesha kwamba mimi ni mbinafsi na kwamba ninapokea rushwa
ili kukihujumu chama changu. Nitazianisha tuhuma kwa kifupi na kuzijibu
kama ambavyo nimekuwa nikizijibu katika vikao mbalimbali vya chama.
i) Tuhuma kwamba sikushiriki kumpigia kampeni mgombea wetu wa urais
katika uchaguzi wa mwaka 2010. Ningependa kueleza yafuatayo kuhusu
jambo hili:
Mimi nilikuwa mgombea wa ubunge katika Jimbo la Kaskazini huko Kigoma.
Pamoja na kuwa mgombea wa ubunge, nilifanya kampeni katika
majimbo mengine 16 katika mikoa mbalimbali, ikiwemo Dar es Salaam,
Mtwara, Pwani, Shinyanga, Mara na Rukwa. Hakuna kiongozi yeyote wa juu
aliyefanya kampeni katika majimbo mengi kama mimi, ukiacha mgombea
urais.
Kote nilipopita nilimpigia kampeni wagombea wetu wa udiwani, ubunge na Rais.
Katika Mkoa wa Kigoma nilizunguka na mgombea urais katika kata
zote za Kigoma Kaskazini na majimbo yote manane ya Mkoa wa Kigoma.
ii) Tuhuma kwamba katika Mkoa wa Kigoma nilishindwa kuwapigia
kampeni wagombea wetu kiasi kwamba peke yangu ndiye niliyeshinda katika
uchaguzi huo. Ukweli ni kwamba niliwapigia sana kampeni wagombea wetu,
na hivyo ndivyo wapiga kura wa Kigoma walivyoamua.
iii)
Tuhuma kwamba nilishiriki kuwashawishi wagombea wetu katika baadhi ya
majimbo kujitoa katika uchaguzi wa mwaka 2010 ili kuwapisha wagombea wa
CCM wapite bila kupingwa kwa njia ya rushwa. Majimbo yanayotajwa ni
pamoja na Sumbawanga, Musoma Vijijini na Singida Mjini. Kama
nilivyokwisha kueleza katika vikao mbalimbali vya chama jambo hili si la
kweli na hakuna popote ambapo watoa tuhuma hizi wamewahi kutoa ushahidi
kwamba nilifanya jambo hili. Nipo tayari kwa uchunguzi ndani ya chama
na watoa tuhuma waje na ushahidi bayana wa jambo hili. Si afya kwa chama
kuendelea kurudiarudia tuhuma hizi kila mara tangu mwaka 2010 bila
uchunguzi wowote kufanyika na jambo hili lifikie mwisho.
iv) Tuhuma kwamba nimekuwa sishiriki katika operesheni mbalimbali za
chama: Ukweli ni kwamba nimeshiriki sana katika operesheni mbalimbali za
chama ndani na nje ya nchi. Kwa mfano, mwaka 2011 tulikuwa na
operesheni kubwa katika mikoa ya Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na
nilikwenda katika mikoa yote tuliyotembelea. Mwaka 2012 baada ya hoja ya
mkonge bungeni nilifanya ziara Mkoa wa Tanga. Mwaka 2012 kulikuwa na
operesheni kubwa moja katika mikoa ya kusini ya Mtwara na Lindi.
Operesheni hii sikushiriki kwa sababu nilikuwa nchini Marekani kufungua
matawi kwa mwaliko wa Watanzania wanaoishi huko.
v) Tuhuma
kwamba nimekidhalilisha chama kwa tamko la PAC kwamba Hesabu za Vyama
hazijakaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG):
Katika jambo hili ninatuhumiwa kwamba mimi kama Naibu Katibu nilipaswa
kuwasiliana kwanza na viongozi wa chama 'kuwatonya' ili wajiandae.
Kwamba kutokuwatonya kumekidhalilisha chama na kukiweka kundi moja na
CCM na nastahili kuadhibiwa vikali kwa kuwa katika taarifa yangu
nilikuwa na nia mbaya na chama chetu. Maelezo yangu niliyoyatoa na
ambayo ningependa kuyakariri hapa kuhusu jambo hili ni kama ifuatavyo:
Utawala bora hautaki mimi kutumia nafasi yangu ya uenyekiti wa
PAC kulinda chama changu na kuonea vyama vingine. Kufanya hivyo ni
kuendeleza tabia zile zile ambazo tunazipinga na ambazo tunapigania
kuzibadilisha
Napenda kusisitiza kwamba hakuna chama ambacho
kimewahi kukaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG).
Natambua kwamba mahesabu ya chama changu yamekuwa yakikaguliwa na
wakaguzi wa nje kwa utaratibu tuliojiwekea. Lakini matakwa ya kisheria
ni kwamba mahesabu ya vyama vya siasa hayajakaguliwa na CAG, na hili ni
kosa la kisheria, bila kujali kosa hili ni la nani.
vi) Tuhuma kwamba mimi ni mnafiki katika kukataa kwangu kuchukua Posho za Vikao
Mtakumbuka kwamba mimi nilikataa kuchukua posho tangu mwaka 2011
kama ishara ya kuonyesha kwa vitendo msimamo wa chama chetu wa kupinga
posho za kukaa na matumizi mengine yasiyofaa katika fedha za umma kama
ilivyoanishwa kwenye Ilani yetu ya mwaka 2010-2015. Mtakumbuka kwamba
hivi karibuni Mheshimiwa Lema amenishutumu kwamba kukataa kwangu
kuchukua posho ni unafiki kwa sababu ninapokea posho kubwa zaidi katika
mashirika ya umma ambapo mimi ni mwenyekiti wa kamati husika. Ninapenda
kueleza yafuatayo kuhusu jambo hili:
Sipokei posho
yeyote ya vikao (sitting allowance) ndani na nje ya Bunge tangu mwaka
2011. Hii ni pamoja na vikao vyote katika Kamati za Bunge
ninavyohudhuria. Mtu yeyote mwenye ushahidi vinginevyo auweke hadharani.
Swala la kukataa posho (sitting allowance) ni swala la kiilani
katika chama chetu, na kwangu ni swala la kimisingi zaidi. Katika Wilaya
yangu vifo vya kina mama wajawazito ni 1900 kati ya wanawake 100,000
wenye ujauzito. Vifo hivi vinatokana na ukosefu wa huduma kwa sababu ya
bajeti finyu. Ndiyo maana nilifurahi sana kwa chama chetu kuliweka swala
la kupunguza matumizi ya Serikali katika Ilani, na kuondoa posho za
wabunge, ambao tayari wanapokea mishahara mikubwa, kungesaidia sana
kupatikana fedha ambazo zingeokoa vifo vingi vya kina mama.
Jambo hili si suala la ugomvi baina yangu na Mheshimiwa Lema. Ni suala la msingi katika chama chetu.
3. Usambazaji wa Ripoti ya Siri kuhusu Zitto Kabwe
Hivi karibuni kulisambazwa waraka unaoitwa ripoti ya siri kuhusu
mimi ukibeba lundo la tuhuma kwamba nimehongwa fedha nyingi ili
kukihujumu chama changu. Waraka huu ulidaiwa kuwa umechomolewa kutoka
makao makuu ya CHADEMA. Jambo hili pia lilijadiliwa katika kikao cha
juzi kwa kifupi, na majibu ya viongozi wa chama ilikuwa ni kwamba waraka
huu haukuandaliwa wala kusambazwa na makao makuu. Katika mchango wangu
nililalamikia mambo matatu yafuatayo:
Kwamba baadhi ya
waliokuwa wanasambaza waraka ule walikuwa ni viongozi wa chama chetu.
Bahati mbaya hadi leo hakuna hata mmoja ambaye amekwishachukuliwa hatua
za kinidhamu. Ninaamini kwamba kuna siku watu hao watachukuliwa hatua
kwa mujibu wa taratibu za chama chetu.
Kwa kuwa chama
kimekana rasmi kuhusika na waraka huu, nitaendelea na taratibu za
kisheria ili kuhakikisha kwamba wote waliohusika kutengeneza hekaya ile
wanachukuliwa hatua stahiki za kisheria.
4. Hitimisho
Ninatambua kwamba kuna watu walitegemea leo ningejibu mapigo na
ningewazodoa watu kwa majina kama ilivyo kawaida katika siasa za
Tanzania. Natambua pia kwamba, kama ilivyo kawaida wakati wa migogoro
katika vyama vya siasa hapa Tanzania, kuna watu walitegemea leo
ningetangaza 'maamuzi magumu'. Natambua kwamba wapo ambao wangependa
kupata nafasi ya kuendelea kutumia suala hili katika harakati zao za
kudhoofisha mapambano ya demokrasia na uthabiti wa siasa za ushindani
nchini mwetu. Napenda wanachama wa CHADEMA na wapenda demokrasia na
siasa safi wote nchini watambue kwamba mimi bado ni mwanachama mwaminifu
wa chama hiki na nitakuwa wa mwisho kutoka kwenye chama hiki kwa hiari
yangu. Nitafuata taratibu zote ndani ya chama katika kuhitimisha jambo
hili.
Naomba wanachama waelewe kwamba mimi kama binadamu
ninaumia ninapopigwa. Tuhuma ninazorushiwa ni kubwa na zinanikwaza.
Tuache siasa za uzushi ili tujenge chama chetu na nchi yetu, ili
hatimaye tuwakomboe Watanzania wenye matarajio na imani kubwa kwa chama
chetu.
Kama mwanasiasa kijana niliyekaa katika siasa kwa
muda sasa yapo mengi mazuri nimeyafanya. Lakini kuna maeneo nilipojikwaa
na yapo makosa niliyofanya kisiasa katika maisha yangu ya siasa.
Kinachoendelea ndani ya chama chetu ni mapambano ya kukuza
demokrasia. Ni mapambano baina ya wapenda demokrasia dhidi ya
wahafidhina, waumini wa uwajibikaji dhidi ya wabadhirifu na wapenda
siasa safi dhidi ya watukuzao siasa majitaka. Hii ni changamoto kubwa
ndani ya chama chetu inayohitaji uongozi shupavu kuikabili. Nitasimama
daima upande wa demokrasia. Kama alivyopata kunena mmoja ya wanasiasa
maarufu, 'kiwango cha juu kabisa cha uzalendo katika nchi ni kukubali
kutofautiana kimawazo', na ninatamani huu ndio uwe utamaduni wa chama
chetu.
Kabwe Zuberi Zitto, Mb
Dar es Salaam.
24 Novemba, 2013
No comments:
Post a Comment