Thursday, October 10, 2013

POSTA WAZINDUA HUDUMA MPYA YA CITY URGENT MAIL MJINI DODOMA(pCUM)


Mkuuwa mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi amelitaka shirika la posta Mkoa wa Dodoma kuhakikisha wananchi wa kawaida wanafikiwa na huduma mpya ya posta ya haraka ya kukusanya na kusambaza nyaraka, vipeto na vifurushi mjini Dodoma inayofahamika kama City Urgent Mail-pCUM ili jamii kuanzia ngazi ya mwananchi wa kawaida ifaidike na huduma hiyo.

Dr Nchimbi aliyasema hayo mapema leo hii kwenye viwanja vya ofisi za posta mjini Dodoma wakati wa maadhimisho ya siku ya posta duniani  yaliyokwenda sambamba na uzinduzi wa huduma hiyo mpya ya posta. Dr. Nchimbi alilitaka shirika la posta kutowatazama makampuni makubwa pekee ya kibiashara,taasisi za serikali,mashirika na wafanyabiashara wakubwa bali wahakikishe huduma hiyo inawafikia hadi wananchi wa kawaida kwani huduma hiyo ina umuhimu wa kipekee kwa makundi hayo yote.

Aliongeza kuwa wakati umefika wa shirika la posta kuingia mashirikiano na mashirika/makampuni/taasisi zinazotoa huduma kwa jamii kama mabenki, kampuni za simu, mamlaka za maji safi na salama na nyinginezo ili kuongeza ufanisi katika kuwahudumia wananchi. Alisema kuwa kwa kiasi kikubwa huduma hii inarahisisha utendaji,inaokoa muda na hivyo inaongeza ufanisi na tija katika kutoa huduma kwa watu.

Dr Nchimbi pia aliwasisitiza wananchi w mkoa wa Dodoma wajasiriamali,taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za serikali kuichangamkia huduma hiyo kwani ni ya gharama nafuu,inaokoa muda na kuleta ufanisi na iko wazi kwa mtu wa aina yoyote na shughuli za aina yoyote ya halali. Katika hatua nyingine aliwaagiza mamlaka ya mawasiliano TCRA Mkoa wa Dodoma, kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauriya Manispaa ya Dodoma na Mamlaka ya ustawishaji makao makuu chini ya uongozi wa ofisi ya mkuu wa wilaya Dodoma Mjini kuona namna ya kukamilisha anuani za mitaa na namba za majengo ili huduma hiyo mpya ya posta iweze kufanyika kwa ufanisi mkubwa.

Kwa upande wake meneja wa posta mkoa wa Dodoma Bi. Margreth Mlyomi aliuambia umma wa wananchi na wadau wa posta mkoa wa Dodoma kuwa posta imekuwa na uzoefu wa kuendesha shughuli zake kwa usiri mkubwa wa nyaraka na mizigo mbalimbali n a hivyo huduma hii mpya ya pCUM itazingatia sana usiri na ufanisi hususani wa muda na hivyo wadau waichangamkie.

Nae meneja wa huduma ya barua za haraka-EMS kutoka posta makao makuu Ndg. John Tinga alibainisha kuwa huduma hiyo ya pCUM imeanza hapa nchini tangu  mwaka 2004 na hadi sasa inapatikana kwenye baadhi ya  mikoa ikiwemo Dar es salaam, Arusha, Mwanza, Zanzibar na sasa imepiga hodi Mkoa wa Dodoma na kuongeza kuwa maeneo yote ilipotangulia huduma hiyo imeonekana kuleta ufanisi mkubwa



Mkuu wa mkoa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi (wa pili kulia) akikata utepe kuashiria kuzindua huduma ya posta ya haraka ya ukusanyaji na usambazaji  nyaraka, vipeto na vifurushi mjini Dodoma (city urgent mail-pCUM). Hafla hiyo ya uzinduzi ilifanyika mapema leo hii kwenye viwanja vya ofisi za posta mjini Dodoma, wengine ni meneja wa posta Dodoma Bi. Magreth Mlyomi (kulia) na meneja wa huduma ya barua za haraka EMS makao makuu Ndg. John Tinga

Mkuu wa mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi (kulia) akimkabidhi afisa masoko wa posta Dodoma Ndg. Michael Mwanachuo moja ya pikipiki itakayotumika  kutoa huduma ya haraka ya kukusanya na kusambaza nyaraka, vipeto na vifurushi mjini Dodoma- pCUM.

No comments:

Post a Comment