Tuesday, October 8, 2013

KIWANGO CHA WADAHILIWA CHUO KIKUU CHA DODOMA(UDOM) KINASHUKA KILA MWAKA KUTOKANA NA KUKOSA VIGEZO.

                                                                                   
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha DOdoma  UDOM Prof. Idris Kikula amebainisha kuwa changamoto ya ukosefu wa wahitimu  wa kutosha wenye vigezo vinavyokidhi kudahiliwa kujiunga na kozi mbalimbali chuoni hapo imesababisha kushuka kwa idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa chuoni hapo mwaka hadi mwaka.

Hayo yalisemwa  mapema leo hii wakati wa sherehe za uzinduzi wa  baraza la pili la wafanyakazi wa chuo kikuu cha Dodoma zilizofanyika kwenye ukumbi wa SENETI chuoni hapo. Prof. Kikula ambaye pia ndio mwenyekiti wa baraza hilo la wafanyakazi chuoni hapo amesema mbali na changamoto ya kushuka kwa idadi  ya wanafunzi wanaodahiliwa chuoni hapo, chuo kinakabiliwa na ufinyu wa bajeti unaotokana na vyanzo vichache vya mapato na  ufinyu wa ruzuku ya serikali  na hivyo chuo kinakuwa na wakati mgumu wa kufikia malengo yake.

Aidha, ili kukabiliana na changamoto hizi, chuo kimefanya jitihada za makusudi kwa kuanzisha programu za cheti na diploma kuanzia mwak huu wa masomo lengo likiwa kuongeza wigo wa udahili wanafunzi na pia kipato na kwa mujibu wa Prof. Kikula tayari kwa mwaka huu wa kwanza tangu programu hizi zianzishwe , chuo kimeshadahili wanafunzi 494  katika programu hizi mpya.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi wakati akizindua baraza la pili la wafanyakazi chuo kikuu cha Dodoma amelitaka baraza hilo kwakuwa linaundwa na wajumbe ambao ni wanazuoni kuhakikisha linajenga utamaduni wa kuishauri menejimenti ya chuo ipasavyo juu ya njia mbadala za kutatua changamoto zilizopo chuoni hapo na hata kuishauri serikali juu ya namna ya kutatua matatizo yanayovikabili vyuo vikuu na elimu ya juu hapa nchini.

Dr. Nchimbi aliomgeza kuwa uzoefu unaonesha pale mabaraza ya wafanyakazi yanapotumika vizuri yanasaidia sana kutatua changamoto mbalimbali, kuleta maelewano mahala pa kazi na kuongeza tija na hivyo kuagiza uongozi wa chuo ikuu  cha Dodoma kwa kushirikiana na baraza hilo la wafanyakazi  kuhakikisha kuwak kero ya madai mbalimbali ya wafanyakazi yanashughulikiwa tena kwa kufuata sheria kanuni na taratibu zilizopo, aidha ameliagiza baraza hilo la wafanyakazi UDOM kuhakikisha linafanya vikao vyake vinavyotakiwa kufanywa kisheria  na pia kujiepusha na migogoro.

Picha ya pamoja kati ya mkuu wa mkoa Dodoma Dr. Rehema Nchimbi, Uongozi wa chuo kikuu cha Dodoma na wajumbe wa baraza la pili la wafanyakazi chuoni hapo muda mfupi baada ya  mkuu wa mkoa kulizundua baraza hilo  mapema leo hii..
                                                      


                  



No comments:

Post a Comment