*Ni ya uchunguzi uliofanywa na Mkemia Mkuu wa Serikali
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepokea taarifa rasmi ya uchunguzi wa kifo
cha Faru John kutoka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali, Prof. Samwel Manyele
ambaye alikuwa akiongoza tume maalum iliyoundwa na Waziri Mkuu.
Waziri Mkuu amepokea taarifa hiyo, leo (Jumatatu, Machi 27, 2017) kwenye
ukumbi wa mikutano wa Ofisi ya Waziri Mkuu, Magogoni jijini Dar es
Salaam.
Akisoma taarifa hiyo mbele ya Waziri Mkuu, Prof. Manyele amesema tume
yake ilifanya uchunguzi wa kifo cha Faru John kwa kupima vinasaba vya
sampuli mbalimbali vikiwemo mzoga, fuvu, mifupa, pembe, damu, ngozi na
kinyesi kilichokaushwa ambapo ilibainika kuwa vyote ni vya mnyama mmoja,
aina ya faru mweusi ambaye ni dume.
Prof. Manyele amesema matokeo hayo yamethibitisha kuwa faru John alikufa
katika hifadhi ya Sasakwa Grumeti kwa kukosa matunzo na uangalizi wa
karibu.
“Maabara iliyotumika ni ya Chuo Kikuu cha Pretoria, Afrika Kusini chini
ya usimamizi wa timu ya wataalamu kutoka Tanzania, wachunguzi wa
Serikali, chini ya Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali.
Sababu za kifo chake zilichangiwa na kukosa matunzo na uangalizi wa
karibu, kukosa matibabu alipoumwa, mazoea yanayotokana na kutofuata
taratibu zilizowekwa kisheria na mapungufu ya kiuongozu kwa Wizara
husika, hifadhi na taasisi zake,” amesema.
Prof. Manyele amesema mapungufu waliyoyabaini kutokana na uchunguzi huo
ni kutokuwepo kwa kibali rasmi cha kumhamisha Faru John; kukosekana kwa
mkataba wa kupokelewa kwa Faru John hifadhi ya Sasakwa Grumeti na
kutofuatiliwa kwa afya na maendeleo ya Faru John baada ya kuhamishwa.
Mengine ni uchukuaji holela wa sampuli za wanyama pori kwa lengo la
utafiti na kuzisafirisha nje ya nchi; migongano ya kimaslahi kati ya
watumishi waliolenga kusimamia taratibu na wale wenye kusimamia maslahi
binafsi na uwepo wa taasisi nyingi zenye mamlaka sawa juu ya masuala ya
uhifadhi wa wanyamapori.
“Pamoja na kwamba mawasiliano yanaonyesha zoezi hilo liliridhiwa na
Wizara, hapakuwepo na kibali rasmi kutoka kwa Mkurugenzi wa Wanyamapori
cha kuruhusu kumhamisha Faru John kutoka NCAA kwenda Grumeti,” amesema
Prof. Manyele katika ripoti yake.
Akizungumzia kuhusu uchukuaji holela wa sampuli za wanyama pori kwa
lengo la utafiti na kuzisafirisha nje ya nchi, Prof. Manyele amesema
kumbukumbu za watafiti na aina ya sampuli wanazochukua haziwekwi vizuri
na kwamba tume inashauri TAWIRI na TANAPA wapewe msisitizo juu ya
umuhimu wa kuzingatia majukumu yao.
Amesema kuna umuhimu wa kudhibiti watafiti na tafiti ili kulinda taarifa
muhimu za vinasaba vya wanyamapori (Genetic information) dhidi ya
mataifa mengine.
“TUME inashauri maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali ianzishe kitengo cha
Sayansi Jinai na Uchunguzi wa Vinasaba vya Wanyamapori (DNA Forensic
Wildlife Laboratory) ili Serikali na vyombo vyake iweze kufanya maamuzi
mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupata ushahidi wa kimahakama katika kesi
za jinai zinazohusu wanyamapori (Expert Witness).
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kusomewa ripoti huyo,
Waziri Mkuu aliishukuru timu ya uchunguzi iliyokuwa chini ya Mkemia Mkuu
wa Serikali kwa kazi iliyoifanya ikiwemo kuainisha udhaifu uliokuwemo
ndani ya Wizara ya Maliasili na Utalii na taasisi zake.
“Ofisi yangu itaipitia taarifa hii ambayo ni kubwa kiasi na kuifanyia
kazi. Matokeo ya kazi hiyo, tutayatoa hivi karibuni ili kuonyesha
Serikali imeamua kufanya nini juu ya mapendekezo yaliyotolewa.”
Alimtaka Mkurugenzi Msaidizi wa Kitengo cha Kupambana na Ujangili wa
Wanyamapori, Bw. Robert Mande, afuatilie mapendekezo yaliyoainishwa na
tume hiyo na wayafanyie kazi mapema iwezekanavyo.
Waziri Mkuu aliiunda tume hiyo Desemba 10, mwaka jana baada ya kupokea
pembe mbili za faru John na taarifa yenye nyaraka zilizotumika
kumhamisha faru huyo.
Hatua hiyo ilifuatia agizo alolitoa Desemba 6, 2016, akiwa ziarani
mkoani Arusha, ambapo alitoa siku mbili na kuutaka uongozi wa Mamlaka ya
Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), umletee nyaraka zote zilizotumika
kumhamisha faru John kutoka kwenye hifadhi hiyo.
Alitoa agizo hilo alipotembelea ofisi za makao makuu ya NCAA zilizoko
wilayani Ngorongoro, mkoani Arusha na kuzungumza na watumishi wa mamlaka
hiyo pamoja na Wajumbe wa Baraza la Wafugaji ikiwa ni sehemu ya ziara
yake ya kikazi mkoani humo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMATATU, MACHI 27, 2017
No comments:
Post a Comment