Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda akihojiwa Leo mbele ya kamati ya bunge
Na Ofisi ya bunge, Dodoma
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda leo amehojiwa na Kamati
ya Bunge ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge kuhusiana na tuhuma za
kuingilia haki, uhuru na madaraka ya Bunge.
Mhe. Makonda aliwasili Bungeni Dodoma majira ya saa nne asubuhi
kuitikia wito wa Kamati hiyo uliotokana na Azimio la Bunge lililotolewa
na Bunge, Februari 8, 2017 katika Kikao cha Nane cha Mkutano wa Sita
wa Bunge ambapo amehojiwa na kamati hiyo kwa muda wa masaa matatu kuhusu
tuhuma zinazomkabili.
Katika kikao hicho, Bunge liliazimia kwamba Mkuu wa Mkoa wa Dar es
Salaam, Mhe. Makonda na Mkuu wa Mkoa wa Arumeru, Mhe. Alexander Mnyeti
kuitwa mbele ya Kamati ya Bunge ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge
baada ya Bunge ili kujibu tuhuma hizo.
Akizungumza mara baada ya Kamati hiyo kumaliza kazi yake, Mwenyekiti wa
Kamati ya Kamati ya Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, Mhe. George
Mkuchika alisema Kamati hiyo imekutana leo baada ya kuagizwa na
Mheshimiwa Spika wa Bunge kwa mujibu wa Kanuni za Kudumu za Bunge.
“Tumefanya kikao hiki cha Kamati baada ya kuagizwa na Mhe. Spika kwa
kuwa kwa Mujibu wa Kanuni zetu, Kamati hii inakutana pale tu inapoagizwa
na Spika wa Bunge,” alisema.
Alisema Mhe. Spika aliiagiza Kamati hiyo imuite Mhe. Makonda mbele ya
Kamati kufuatia azimio hilo la Bunge lililopitishwa na Bunge Februari
8, ambapo pamoja na mambo mengine Mkuu huyo wa Mkoa alitakiwa kufika
mbele ya Kamati kujibu tuhuma hizo zinazomkabili.
Alisema kwa mujibu wa Azimio hilo, Mhe. Makonda alidaiwa kutoa kauli
kupitia Televisheni ya Clouds akidai kwamba wabunge wanasinzia Bungeni
jambo lililoonekana kwamba ni kudharau Bunge.
“Napenda kutoa taarifa kwamba Mhe. Makonda leo amekuja mbele ya Kamati
na ametupa ushirikiano mzuri, tumepokea maelezo yake na Kamati imemaliza
kazi yake,” alisema.
Alisema kama ilivyo utaratibu, Kamati yake itakabidhi taarifa yake kwa
Mhe. Spika kwa mujibu wa Kanuni ambapo Spika ndiye atakaeamua namna ya
kutoa raarifa kuhusu kazi ya Kamati hiyo.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment