Na. Immaculate Makilika- MAELEZO
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne Mhe.
Dkt. Jakaya Kikwete amesema kuwa anapenda kuendelea kufanya shughuli
zinazosaidia kuleta maendeleo kwa watu na jamii.
Akizungumza na waandishi wa
habari leo Jijini Dar es salaam, wakati alipokuwa akizindua Taasisi
yake ya Jakaya Kikwete (Jakaya Mrisho Kikwete Foundation) alisema kuwa
kwa muda mrefu amekua akipenda na kujihusisha na shughuli mbalimbali za
maendeleo ya watu na hivyo Taasisi yake itamsaidia katika kufikia
malengo yake.
“Nimetumia muda wangu kwa ajili ya
maendeleo ya watu, baada ya shule, nilikitumikia Chama cha
Mapinduzi(CCM), nilitumikia Jeshi na baadae Serikali, kwangu Taasisi hii
imekuwa chombo kitakachonisaidia kuendeleza maono yangu na kutimiza
ndoto zangu katika kuendelea kusaidia watu” alisema Dkt. Kikwete.
Akiizungumzia taasisi hiyo Kikwete
alisema kuwa, Taasisi yake ina wajumbe 9 kutoka sehemu mbalimbali
duniani wenye nyadhifa na heshima kubwa katika nchi zao.
Ameongeza kuwa Taasisi hiyo
imejikita kusaidia jamii katika maeneo makubwa manne, maendeleo ya
jamii hasa katika kujikita kuondoa umaskini, mabadiliko ya hali ya nchi
na kilimo kwa wakulima wadogo.
Pia Taasisi hiyo imejikita katika huduma za afya, kutokomeza malaria na afya ya mama na mtoto.
Maeneo mengine ambayo Taasisi hiyo
inajihusisha nayo ni ni elimu kwa vijana ili kukuza vipaji vyao na
kuwapa mafunzo kuhusu uongozi bora, usawa wa kijinsia na namna ambavyo
Serikali inavyotoa huduma kwa wananchi.
Aidha, alisisitiza kuwa Taasisi
yake itaisaidia Serikali, mashirika na Taasisi mbalimbali ili
kushirikiana kuwaletea maendeleo watanzania na watu mbalimbali duniani.
Dkt. Kikwete amewataja Wajumbe wa
Bodi ya Udhamini ya Taasisi yake kuwa ni Balozi Ombeni Sefue aliyekuwa
Katibu Mkuu Kiongozi, Profesa Rwekaza Mukandala Makamu Mkuu wa Chuo
Kikuu Cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Willium Mahalu Mhadhiri
Mwandamizi katika Chuo Kikuu cha Tabibu cha Bugando.
Wengine ni Balozi Mwanaidi Maajar
aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Uingereza, Abubakar Bakhresa,
Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Makampuni ya Bakhresa, Genevieve Sangudi
Mtaalamu wa Masuala ya kibishara ya Kimataifa kutoka Marekani.
Pia wapo Dato’ Sri Idris Jala,
Waziri asiyekuwa na Wizara Maalumu nchini Malyasia, Balozi Charles R.
Stith aliyekuwa Balozi wa zamani wa Marekani nchini Tanzania pamoja na
Dkt. Carlos Lopes ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Taaisi ya Mafunzo na
Utafiti ya Umoja wa Mataifa (UNITAR).
Taasisi ya Maendeleo ya Jakaya
Kikwete ilisajiliwa tarehe 17, Februari 2017, na hii ni mara ya kwanza
kwa wajumbe wa bodi ya wadhamini kukutana tangu kuanzishwa kwake.
No comments:
Post a Comment