Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akihutubia wakati wa
uzinduzi wa Ripoti ya nchi kuhusu Mpango wa Hiari wa Nchi za Umoja wa
afrika kujipima kwa Vigezo vya Utawala (APRM). (Picha na Ofisi ya Makamu
wa Rais)
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akionyesha kitabu chenye
ripoti ya nchi kuhusu Mpango wa Hiari wa Nchi za Umoja wa afrika
kujipima kwa Vigezo vya Utawala (APRM) mara baada ya kuzindua taarifa
hiyo kwenye Kituo cha Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere.
Makamu
wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu
Hassan leo amezindua Taarifa ya Nchi kuhusu Mpango wa Hiari wa Nchi za
Umoja wa Afrika kujipima kwa Vigezo vya Utawala (APRM).Uzinduzi huo
ulihudhuriwa na kiongozi wa Jopo la Mchakato huo kwa Tanzania ambaye
pia ni Makamu Mwenyekiti wa Jopo la Watu Mashuhuri Bi. Brigitte Sylvia
Mabandla, Viongozi wengine wa APRM Tanzania ni Balozi Ombeni Sefue,
Profesa Hasa Mlawa na Balozi Aziz Mlima aliyemuwakilisha Waziri wa Mambo
ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki pamoja na baadhi ya Mawaziri
wa Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
APRM
ni mpango wa hiari wa kujipima kwa vigezo vya utawala bora uliobuniwa
mwaka 2003 na Wakuu wa Nchi na Serikali wa nchi wanachama wa Umoja wa
Afrika. Lengo la mpango huu ni kuziwezesha nchi wanachama kujitathmini
kwa vigezo vya utawala bora katika maeneo manne ambayo ni; Demokrasia na
Utawala wa Kisiasa; Usimamizi wa Uchumi; Utendaji wa Mashirika ya
Biashara; na Maendeleo ya Kijamii na Kiuchumi.
Akihutubia
katika uzinduzi huo, Makamu Rais amewapongeza Wakuu wa Nchi na Serikali
wanaoshiriki katika mchakato wa APRM kwa ujasiri wao wa kushirikishana
taarifa za kuaminika kuhusu masuala ya utawala bora katika nchi zao.
“Taarifa hizi zinaonesha wazi juu ya hali ya utawala bora katika Bara
letu na kutupa nafasi ya kujirekebisha pale ambapo kuna dosari na
kujipongeza pale tunapofanya vizuri na kuwapa wengine nafasi ya
kujifunza zaidi’’ alisema Makamu wa Rais.
Aidha
alisisitiza kuwa kupitia utaratibu huu tumeweza kuuonesha ulimwengu
nguvu zetu za pamoja kama Bara la Afrika katika kuboresha demokrasia,
amani na utulivu, utawala wa sheria na utawala bora kwa ujumla.
Kwa
upande wa Tanzania, Makamu wa Rais alisema mchakato huu unatuonesha na
kutukumbusha falsafa na maono ya Hayati Baba wa Taifa Mwl. Nyerere
(Tujisahihishe, 1962) na Mwongozo wa TANU wa mwaka 1971. Alisema nchi
yetu imefanya mambo mengi katika kutekeleza mpango huo ikiwemo
kuimarisha taasisi zinazoshughulikia masuala ya utawala bora ikiwemo
Tume ya Haki za binadamu na Utawala Bora, taasisi ya kuzuia na kupambana
na rushwa na sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma.
Kuhusu
changamoto zilizobainishwa kwenye taarifa husika, Makamu wa Rais
alisema kwa kiasi kikubwa zimepatiwa ufumbuzi katika Mkakati wetu wa
Maendeleo 2025 unaolenga kukuza na kupanua wigo wetu wa uchumi ili kuwa
nchi ya uchumi wa viwanda. Kuhusu suala la Muungano alisema muundo wa
Muungano wetu ni wa serikali mbili ambazo ni Serikali ya Jamhuri ya
Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Makamu
wa Rais alisema miongoni mwa maeneo ya vipaumbele katika mchakato wa
kuelekea kuwa nchi ya viwanda ni kuimarisha sekta ya nishati na umeme.
“Kwa ujumla tumefanya jitihada kubwa katika huduma ya nishati kutokana
na ugunduzi mkubwa wa gesi asilia hapa nchini” alisisitiza Makamu wa
Rais. Kwa sasa umeme unasambazwa kwa kasi katika vijiji vyetu kupitia
Wakala wa Nishati Vijijini (REA).
Serikali
imefanya jitihada kubwa katika kuzipatia ufumbuzi changamo za kijamii
kama vile elimu, afya na maji ambazo zilitajwa kama vikwazo katika
taarifa husika. Aidha, Serikali imeongeza uandikishaji wa wanafunzi kwa
shule za msingi na sekondari, imeboresha mazingira ya kujifunzia na
kufundishia, imejenga madarasa na maabara, imeboresha maslahi ya walimu
na kuhakikisha inajenga vyuo vya ufundi katika kila wilaya.
Pia
Makamu wa Rais alisema Tanzania inatambua kuwa mchakato huu wa APRM ni
endelevu hivyo serikali itaendelea na jitihada zake kuhakikisha kwamba
changamoto zote zilizobainishwa ndani ya taarifa zinapatiwa majawabu
kupitia serikali na taasisi zake, asasi binafsi na wananchi kwa ujumla.
Mwisho,
alishukuru na kutambua mchango wa washirika wa maendeleo katika
kufadhili kazi za APRM na kuwaalika kuendelea kuchangia shughuli za
APRMTanzania ikiwemo mpango kazi wa Taifa.
No comments:
Post a Comment