Mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Jijini Dar es salaam Ndg John Lipesi
Kayombo ameungana na wakurugenzi wengini nchini kuhudhuria Mkutano wa
Uzinduzi wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini uliofanyika Kwenye
Ukumbi wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere uliopo katika Chuo Cha
Mipango Mjini Dodoma Leo Julai 2, 2017.
Mkurugenzi Kayombo ameshiriki Mkutano huo uliofunguliwa na Waziri
Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Kassim M. Majaliwa (MB)
wenye dhamira ya kuleta mageuzi makubwa katika sekta ya Barabara nchini
kutokana na kuanzishwa kwa wakala wa barabara Mijini na Vijijini.
Uanzishwaji wa Wakala wa Barabara nchini ni utekelezaji wa ilani ya
uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Mwaka 2015 iliyopo katika
ukurasa wa 54 inayoielekeza serikali kuanzisha Wakala/Taasisi
itakayosimamia kazi za ujenzi na matengenezo ya barabara za Halmashauri,
Miji, na Majiji ambazo zipo chini ya TAMISEMI ifikapo mwaka 2020.
Katika Mkutano huo zimeelezwa changamoto mbalimbali zinazozikabili
mamlaka za serikali za Mitaa katika ujenzi, ukarabati na matengenezo ya
miundombinu ya Barabara ambazo ni pamoja na Miradi kutekelezwa kwa
viwango duni, Ucheleweshaji wa utekelezaji wa miradi kutokana na mipango
isiyoridhisha, Kandarasi kutolewa bila kuzingatia vigezo, uwezo na
sifa.
Changamoto zingine ni pamoja na kutokuwepo kwa viwango
vinavyoshabihiana vya ubora wa barabara Kati ya Halmashauri Moja na
nyingine, Fedha zilizopangwa kutekeleza miradi ya barabara kutotumika
kutokana na urasimu wa viongozi wa Halmashauti, Rushwa iliyokithiri
katika utoaji wa zabuni, Mgongano wa maslahi na usimamizi hafifu wa
mikataba ya ujenzi.
Wakala huu utasaidia kuimarisha mtandao wa barabara za vijijini na
hivyo kuwawesesha wananchi wengi zaidi kusafiri na kusafirisha bidhaa za
mashambani kwa urahisi.
Katika Mkutano huo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe
Majaliwa K. Majaliwa akizungumza kabla ya kuzindua Wakala wa Barabara
Mijini na Vijijini alieleza manufaa yatakayopatikana kutokana na kuwa na
Barabara za Vijijini na Mijini kuwa ni pamoja na kuongeza chachu ya
uzalishaji Mali mashambani kutokana na urahisi wa kufikisha mazao
sokoni, Kushusha bei ya vyakula mijini kutokana na gharama za
kusafirisha mazao kutoka mashambani kupungua.
Mengine ni kuboresha na kubadili hali za kimaisha na kiuchumi kwa
wananchi, kufanya maeneo mengi zaidi ya nchi kufikika kwa urahisi na
hivyo kuboresha utoaji wa huduma za kijamii na Kutoa ajira kwa vijana
katika maeneo ambayo ujenzi au ukarabati wa miundombinu utakapokuwa
unafanyika.
Katika Mkutano huo Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo, imewakilishwa
na Mkurugenzi Kayombo ambaye ameambatana na Kaimu Mkuu wa Idara ya
Ujenzi na Zimamoto Manispaa ya Ubungo Ndg Goodluck Mbanga.
No comments:
Post a Comment