Jonas Kamaleki- MAELEZO
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania,Dkt. John Pombe Magufuli kesho atazindua Pasipoti Mpya ya
Tanzania ya kielektroniki jijini Dar es Salaam.
Uzinduzi huo utafanyika Jumatano,
Januari 31, 2018 kuanzia saa moja na nusu asubuhi, Makao Makuu ya Idara
ya Uhamiaji, Kurasini Dar es salaam.
Hayo yamesemwa na Mrakibu wa
Uhamiaji ambaye pia ni Msemaji Mkuu wa Idara ya Uhamiaji, Ali Mtanda
katika mahojiano maalum na Idara ya Habari (MAELEZO).
Mtanda amesema kuwa Pasipoti Mpya
ya Tanzania ya kielektroniki ni sehemu ya Mfumo wa Uhamiaji Mtandao
ambao utakuwa na visa, vibali mbali mbali na manejimenti mipakani.
Kwa kuwa teknolojia inazidi kukua, Tanzania haiwezi kubaki nyuma ndiyo maana imeamua kuingia katika masuala ya digiti.
Uzinduzi huu utahudhuriwa pia na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali Mohamed Shein.
Marais wastaafu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, waheshimiwa, Ali Hassan Mwinyi, Benjamin William
Mkapa na Jakaya Mrisho Kikwete na viongozi wengine wa Serikali
wanatarajiwa kuhudhuria uzinduzi huo kwa mujibu wa Mtanda.
Tanzania imekuwa mstari wa mbele
katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati katika kutoa huduma zake kwa
wananchi kwa njia ya mtandao. Ikumbukwe kuwa usajili wa makampuni chini
ya Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) wamezindua usajili wa
makampuni kwa njia ya mtandao, miamala ya pesa inafanyika kwa kiwango
kikubwa kwa njia ya mtandao na kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi
ikiwepo kulipa kodi mbali mbali.